KAMA UNADHANI KUNA KITU UNAFICHWA NA MATAJIRI, SAHAU KUHUSU UTAJIRI.

 nilisema kwamba "Ishara ya umasikini mbaya sio ule unaowakosesha watu pesa na mlo wa siku, ila ni ule unaowakosesha watu raha kwenye mafanikio ya wengine." 

Tarehe 15/08/2024 saa 2:05 asubuhi nikasema tena "Kinachochelewesha maendeleo ya masikini wengi sio ugumu wa kupata pesa, ila ni ile tabia ya kupoteza muda kufuatilia maendeleo ya watu wengine."

Na tarehe 17/08/2024 saa 3:21 asubuhi nilisema tena kwa nukuu mbili mfululizo kwamba  
"Hatutofautiani vitu vingi na watu wanaofanya makubwa kwenye hii dunia, ila maarifa na taarifa tulizo nazo ndiyo zinazoamua tujione wa viwango gani na tunaelekea wapi kimaisha." 
Na nukuu ya pili ilisema "Kama ambavyo nyanya moja mbovu huozesha tenga zima vikiwa pamoja, ndivyo ambavyo watu walioshindwa mambo mengi kwenye maisha yao hupambana kuwakatisha tamaa wengine."

Nukuu hizo zinasadifu hoja mbalimbali ambazo watu wengi wamekuwa wakizitoa kwenye mahojiano ya matajiri wengi pindi wanaposema walianza na viwango fulani ambavyo wengi huwa tunaamini ni vidogo sana au ni uongo kwa sababu ndivyo viwango tunavyovichezea kila siku kwenye maisha yetu.

Nitamnukuu tajiri mmoja wa hivi karibuni ambaye nilibahatika kufuatilia mahojiano yake kwa ufupi kupitia TBC Online hivi karibuni,

"Nilianza na mtaji usiozidi Sh. 20,000." Huyo ni tajiri Omary Msigwa mmiliki wa kampuni ya usafirishaji ya mabasi na maroli ya Super Feo na Selous, Shule na miradi mingine.

Mbali na Omar wa Super Feo, pia Mmiliki wa Shabiby Line, Mmiliki wa Mak Juice, Millard Ayo, Mwanadada Niffer, Bakhresa nao pia wamewahi kunukuliwa wakisema kwamba wameanzia chini sana na leo hii ni matajiri.

Kwa muda wa vipindi ambavyo wanakuwa wamealikwa au makala wanazokuwa wameandikwa huwa hautoshi wao kusema kila kitu hata kama watapewa juma zima ila watu wengi huwa tunang'ang'ania kwamba HAIWEZEKANI, wanatudanganya.

Hivi hatuamini kwa sababu wengi hatuwezi, au ni dhana tulizojijengea ukijumlisha hofu na ujinga kama alivyosema Robert Kiyosaki ndiyo huwa vinatuponza?

Zifuatazo ni miongoni mwa dhana chache ambazo masikini wengi tumezishilikilia ila kiuhalisia hakuna chochote kinachofichwa isipokuwa sisi ndiyo tunajificha na uhalisia.

MATAJIRI WENGI WANAFICHA NJIA WANAZOPITA

Ukweli tunaodai hausemwi, ni matajiri wangapi wanasema wazi kwamba wao wanakopa au wao ni mawakala wa shetani, au wana waganga wao au wanamiliki majini na bado hatuamini?

Mark Zuckerberg hajawahi kusema wazi kwamba haamini katika Mungu na kuonyesha upande aliopo? Wangapi tulichagua kwenda kujiunga huo upande mwingine?

Mo hajawahi kusema wazi kupitia BBC akihojiwa na salim Kikeke kwamba pamoja na yeye kuwa ndiye tajiri namba 1 Afrika Mashariki na kati lakini pia yeye ndiye mdaiwa namba moja, hili pia ni uongo?

Kama tunaamini wameua au wanatumia njia za kishirikina ni mara ngapi Dotto Magari na Chief Godlove ambao si matajiri wakubwa ila angalau hatuwezi kujifananisha nao wanakiri wazi kwamba wao ni washirikina?

Ni mara ngapi Fred Vunjabei anajiita mkinga mchawi kama wengine tunavyoamini na hatudadisi? Au anatania na inawezekanaje ukawa ni utani ilhali wengi tunaamini kwamba alisemalo mtu ndilo lililoujaza moyo wake?

Hayati Sir. Andy Chande hakuwa tajiri wa kutisha Tanzania ila enzi za uhai wake alikiri wazi kwamba yeye ni Freemasons na akasema yote yaliyostahili kusemwa wazi kuihusu Freemason na kusema cheo chake lakini mpaka leo wengi tupo vilevile na kung'ang'ania kwamba matajiri hawasemi ukweli na kuita watu Freemasons kwa sababu tu wanavaa suti nyeusi.

Subiri kwanza, huenda hunielewi ngoja nikupe mifano hai zaidi

Baadhi ya matajiri wamewahi kufanya makosa na misukule, majini, manyoka na hirizi zao zikaonekana ila bado waliendelea kuwa matajiri na masikini walibaki kuwa masikini pamoja na kujua kwamba siri ya mafanikio yao ni vitu fulani.

Moja ya mfano hai uliowahi kutokea iringa kwa Mama fulani tajiri ambaye sitamtaja jina lake kwa mfanyakazi wake kujisahau kulisha misukule kwa wakati mpaka ikatoka nje na maelfu ya watu wakashuhudia mpaka wakatawanywa na FFU lakini mpaka leo yule mama bado ni tajiri na masikini walioharibu nyumba yake kwa kujifanya wana hasira kali ilhali ilikuwa ni chuki dhidi yake mpaka wakauana kwa kukanyagana wamebaki kuwa vilevile kwenye eneo lilelile huku tajiri akihamia Dar na kuendelea na biashara zake.

Kwa wanaopafahamu na kuishi makambako naamini mmewahi kumshuhudia yule tajiri wa mabasi ambaye naye sitamtaja na nitafurahi pia kama mnaomfahamu msimtaje ambaye aliwahi kurukwa na akili kwa kile kilichodaiwa kwamba alikosea masharti na kutembea uchi tena kwa kushinda kwenye eneo lake lilelile la ofisi na yanapopaki mabasi yake lakini baadae alikaa sawa na sasa anamiliki mabasi makubwa tofauti na Isuzu, Fuso na Costa alizokuwa nazo kipindi hicho. 

Mbona akina Mo wapo wazi na huwa wanavaa waziwazi kaballah za matambiko ya kihindi kwa ajili ya ulinzi kitu ambacho wengi mnakiita hirizi kwa tamaduni zenu na mnakiogopa kwa sababu mmeambiwa hivyo ni vitu vibaya kwenye dini zenu.

Tajiri gani huwa anahangaika kuficha pete na mikufu yenye vito vinavyochagiza utajiri wao, au ni wapi imefichwa elimu ya pete na unajimu, si ni sisi tu na ujinga wetu wa kuita kila kitu ushirikina ndiyo tunaishia kuogopa ogopa kila kitu na kulialia njaa?

MATAJIRI HAWASEMI HASARA

Mbali na hivyo kuna watu wanasema matajiri hawasemi hasara na mambo mengine ambayo hata bila kusemwa huwa tunayaona.

Ni kweli huwa hatuoni mabasi yanavyoanguka? Au ndiyo sisi tunalaumu na kutusi pindi zinapotokea ajali tu ila tukifika salama huwa hatujali kwamba kulikuwa na dereva aliyekabiliana na mambo mengi ya barabarani na usingizi ili tufike salama?

Ni kweli kwamba hatukumsikia Fred Vunjabei akisema wazi kwamba zabuni aliyoshinda Simba sports club iliwahi kumkata pa kubwa kwa kosa dogo tu la uongozi wa SSC kuchelewa kumpa taarifa kwamba wapo mbioni kubadili mdhamini?

Si juzi tu hapa Fred Vunjabei huyohuyo alirusha video fupi ikionyesha anaunguliwa na stoo yake ya kariakoo iliyoteketeza zaidi ya milioni 200?

Ni nani hakuona hasara ya Azam peach kati ya mwaka 2018 - 2019 kwa kuingizwa sokoni kwa bei ambayo ilikosewa na kusambazwa karibia nchi nzima na kusababisha hasara iliyopelekea mpaka leo ishindwe kurudi kwa ukubwa ule? Je hili nalo hatukuliona?

HITIMISHO

Halafu wanaposema wameanzia kiasi fulani sio kwamba ndiyo wametajirikia kiasi hicho, ila katikati ya safari zao kuna ushirikina, majini, mikopo, hisa, uwekezaji, mipigo na matakataka mengi ambayo huwa yapo wazi na masikini pia tunayafanya ila ujinga ndiyo unatufanya tubaki vilevile.

Binafsi kwa matajiri kama Shabiby, Abood, na Omary wa Superfeo na wengine wengi nitawaamini na kuwachukulia kama mfano wa kuiga kwa sababu kwa muda waliotumia kujenga majina na kupambana naona wanastahili kuwa matajiri wakubwa.

Kwa hatua waliyopo sidhani kama wao ndiyo huwa wanawabembeleza wanahisa kuwekeza kwao haijalishi wanaowekeza kwao ni akina nani au kuyafuatafuata mabenki au makampuni ya mabasi yawakopeshe mabasi. 
Kiuhalisia kampuni nyingi za kichina ndiyo huwatumia wao kama mawakala wa mabasi na tunaona matunda yake kiasi kwamba mpaka JWTZ imeamua kuchukua Yutong badala ya Leyland ambazo zilikuwa aibu kutembea mjini kusambaza na kusafirisha wanajeshi.

Waungwana, ni ngumu kuwaamini wengine kama wewe binafsi haujiamini na mbaya zaidi ukiwa unashikilia dhana za kichawi chawi kama vile kuna tajiri amekuwa tajiri kwa kulala tu na kuletewa pesa na misukule.

Muungwana yeyote awaye vyote kuliko wewe, mpe maua yake na kujifunza kwake na ukiona njia zake ni chafu basi hakikisha zako safi zinakufikisha kule ambapo wewe utakuja kuwa tajiri na kuwaambia watu wakakuamini.

Mwisho kabisa naomba tukumbushane kwamba "Hatuwi matajiri kwa kuwachukia matajiri, tunakuwa matajiri kwa kuuchukia umasikini na kukabiliana nao."

 

Comments

Popular posts from this blog

Jinsi ya kumfanya mwenzi wako akupende zaidi kwa limbwata rahisi tu

NAMNA YA UMASIKINI UNAVYOTENGEZWA

NJIA ZA KUWA NA MAFANIKIO KATIKA MAISHA